Beki kisiki wa Yanga na timu ya Taifa Kelvin Yondani amesema maisha yake ya kusakata kabumbu atayamaliza kunako klabu hiyo
Siku za karibuni kumeibuka sintofahamu kumuhusu hasa baada ya kukosekana uwanjani kwa wiki kadhaa jambo liliosababisha kuibuka kwa tetesi kuwa anajiandaa kuondoka Yanga
Hata hivyo Yondani amesisitiza kuwa hafikiri kujiunga na timu nyingine yoyote, atamaliza soka lake Yanga
Yondani ambaye mwaka huu atatimiza miaka 36, amesema Yanga imempa heshima na maisha hivyo anataka awaachie vijana somo zuri la kujifunza
"Nina muda mfupi sana wa kuendelea kucheza mpira, na nitastaafu kwa heshima ili kuwapisha vijana. Yanga ni klabu iliyonipa heshima na maisha kwa maana ya maendeleo. Siku ntakayoondoka Yanga ndio siku ntakayostaafu, soka langu langu litaishia hapa," amesema
Yondani ni beki aliyeweka historia ya kipekee kwenye soka la Tanzania kwani amezitumikia Yanga na Simba kwa muda mrefu
Alianza kuichezea Simba mwaka 2006 na mwaka 2012 aliikacha timu hiyo na kujiunga na Yanga
Amecheza Yanga kwa miaka nane sasa tena akiwa mchezaji muhimu wa kutegemewa
Huenda akafuata nyayo za mkongwe Nadir Haroub ambaye alistaafu msimu uliopita kwa heshima baada ya kuitumikia Yanga kwa miaka 12