Yanga imeendeleza wimbi la ushindi uwanja wa Taifa baada ya kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa katika uwanja huo
Alikuwa ni David Molinga Ndama aliyeihakikishia Yanga alama tatu muhimu baada ya kuifungia bao pekee kwenye dakika ya 50
Krosi murua iliyochongwa kutoka upande wa kulia na Ditram Nchimbi ilitua mguuni kwa Molinga ambaye alifunga bao lake la sita msimu huu
Bao hilo ni matokeo ya shambulizi la kushitukiza lililofanywa na Yanga mpira ukianzia kwa fundi Haruna Niyonzima ambaye amekuwa kwenye kiwango bora tangu aliporejea Yanga mwezi uliopita

Mtibwa Sugar nao walitengeneza nafasi kadhaa ambazo kama sio uhodari wa Metacha Mnata wangeweza kurejea mchezoni
Matokeo hayo yanaifanya Yanga ifikishe alama 31 na kurejea kwenye nafasi ya nne ikiwa imeshuka dimbani mara 16
Mchezo unaofuata ni dhidi ya Lipuli Fc siku ya Jumatano, Februari 05, 2020 na utapigwa uwanja wa Taifa