Uamuzi wa TFF kuagiza kuanza kwa uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa na mlinda lango Ramadhani Kabwili, ni hatua sahihi zinazostahili kupongezwa lakini ni kama wamechelewa kwani tuhuma hizo hazikuanza leo
Msimu uliopita mara kadhaa aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera alitoa tuhuma kuwa viongozi wa Simba walikuwa wakifanya matukio ya kuhonga timu zilizocheza na Yanga ili kuzuia timu hiyo isipate matokeo katika baadhi ya michezo yake
Zahera alieleza kuwa na ushahidi wa taarifa alizokuwa akipatiwa na wachezaji wasamaria wa timu walizokuwa wakicheza nazo ambao wengine waliwahi kuitumikia Yanga miaka ya nyuma
"Wanatoa ahadi ya Tsh Milioni 10 kwa timu zinazotufunga na Tsh Milioni 5 kwa timu ambazo zinapata matokeo ya sare"
"Wanatumia pesa nyingi kununua wachezaji, wanawalipa mishahara mikubwa lakini bado wanatoa hongo kutafuta matokeo, wachezaji hawa wana kazi gani?," alihoji Zahera
Ni bahati mbaya TFF haikuchukua hatua wakati ule lakini haraka imeagiza uchunguzi kwa hili lililozungumzwa na Kabwili jana
Matukio ya rushwa kwenye soka hayakubaliki, kulingana na sheria za FIFA kama tuhuma hizo zitathibitishwa adhabu kubwa ambayo Simba wanaweza kukumbana nayo ni kushushwa daraja