Pamoja na kupoteza mchezo dhidi ya Azam Fc, yapo mabadiliko ambayo kikosi cha Yanga kimeanza kuonyesha
Kocha Luc Eymael amepoteza mchezo wake wa pili tangu ajiunge na Yanga wiki iliyopita, lakini kuna kazi anaonekana anaifanya
Jambo kubwa ambalo liko dhahiri ni kuwa Yanga imeanza kucheza mpira, tatizo limebaki kwenye safu ya ushambuliaji
Kwa miaka ya hivi karibuni ilikuwa sio rahisi kwa Yanga kuwa bora zaidi ya Azam Fc hasa kwenye umiliki wa mpira
Jana kwa mara ya kwanza Yanga ilikuwa bora zaidi ya Azam Fc. Kuna wakati Yanga iliweza kupiga mpaka pasi kumi huku muda mwingi Azam Fc wakiutafuta mpira

Hata bao walilofunga hawakulitengeneza, Ally Mtoni alijifunga katika harakati za kuokoa mpira
Kazi kubwa iliyobaki ni kwa kocha Eymael na benchi lake la ufundi kufanyia kazi safu ya ushambuliaji, timu itengeneze nafasi nyingi na kuzitumia
Matumizi ya mshambuliaji mmoja mbele bado ni tatizo au inawezekana washambuliaji wanaotumiwa sio aina ya washambuliaji wanaopaswa kucheza peke yao mbele
David Molinga ni msumbufu kwa mabeki lakini sio mchezaji anayetulia sehemu moja ndio maana haonekani kuwa na madhara
Ditram Nchimbi na Yikep Gnamien nao hawana tofauti sana na Molinga sio wachezaji wa kusimama peke yao, wanakuwa wazuri wanapocheza sambamba wawili
Pengine Tariq Seif ndiye mchezaji ambaye anaweza kusimama peke yake mbele
Bao alilofunga katika mchezo dhidi ya Biashara United akiwa ameingia kuchukua nafasi ya Molinga lilidhihirisha uwezo wake
Hata hivyo Tariq alikuwa majeruhi na amerejea kikosini juzi, pengine anaweza kutumika mchezo unaofuata dhidi ya Singida United
Kikubwa ni kwa mashabiki na uongozi wa Yanga kumpa muda kocha Eymael kujenga timu
Wakati mwingine ni vyema kuwapa muda wa kutosha makocha kujenga timu bila ya kujali matokeo yanayopatikana
Kwa sasa Yanga imeshabadili makocha watatu na msimu haujafika hata nusu. Hakuna muujiza utatokea hata Eymael akitimuliwa leo na kuletwa kocha mwingine
Mashabiki tumekuwa na kawaida ya kutokuwa wavumilivu na wakati mwingine kuwapa presha viongozi kufanya maamuzi ya hovyo
Hakuna kocha ambaye anaweza kutengeneza timu kwa wiki moja, wote wanahitaji muda
Kocha huyu ni vyema akaachwa mpaka mwishoni mwa msimu na lengo liwe kutengeneza timu bora kwa ajli ya msimu ujao
Kwani ameletwa timu ikiwa imecheza zaidi ya mechi 10 tena akikabidhiwa timu iliyosajili nyota wapya saba
Sidhani kama Eymael anastahili kulaumiwa kutokana na matokeo sasa kwani tatizo halikuanzia kwake
Tatizo lilianzia kwa Zahera, baadae Mkwasa alianza kuiweka timu sawa lakini kulikuwa na ulazima timu kuwa na Kocha Mkuu
Watani zetu Simba waliwahi kukumbwa na changamoto hii, walikosa uvumilivu na wakatimua makocha kila kukicha
Lakini faida kubwa waliyopata ni kucheza misimu mitano mfululizo bila ya ubingwa wala kushiriki michuano ya Kimataifa
Mabadiliko yalitokea walipomuacha Joseph Omog msimu mzima, aliwatengenezea msingi wa timu imara ambao makocha waliofuata wamekuwa na kazi nyepesi kuendeleza