Mshambuliaji Ditram Nchimbi aliyetua Yanga akitokea klabu ya Azam Fc kwenye usajili wa dirisha dogo huenda akakosa fursa wa kucheza mechi ya watani wa jadi dhidi Simba ambayo itapigwa Januari 04 2020 baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuzuia leseni yake
Yanga iliwaombea wachezaji leseni wachezaji wake wazawa ili waweze kucheza mchezo wa jana dhidi ya Biashara United ambapo TFF ilitoa leseni za Tariq Seif na Adeyum Salem lakini ya Nchimbi ikazuiwa
Uongozi wa Yanga umeeleza kushangazwa na uamuzi huo wa TFF kwani wanaamini walifuata taratibu sahihi za kumsajili mchezaji huyo kutoka Azam Fc
"Nchimbi alikuwa mchezaji wa Azam Fc na sio Polisi Tanzania. Tumefuata taratibu kumsajili sasa tunashangaa kwa nini TFF wanazuia leseni yake," alisema Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli
Klabu ya Polisi Tanzania imemuwekea pingamizi Nchimbi ikihitaji kulipwa fedha ambazo wanadai walimlipa baada ya kufikia makubaliano binafsi ili kumtumia msimu mzima
Kaimu Katibu Mkuu wa Polisi Tanzania Frank Lukwaro amesema hawana nia ya kumzuia Nchimbi kucheza Yanga, wanachotaka ni kurudishiwa fedha ambazo mchezaji huyo alichukua kutoka kwao
Jana Nchimbi aliushuhudia mchezo kati ya Yanga dhidi ya Biashara United akiwa benchi
Yanga ilishinda mchezo huo kwa bao pekee lililofungwa na Tariq Seif