Huyo bilionea wa Yanga, Ghalib Mohammed ni kama sasa anafanyia sifa aisee, kwani unaambiwa wakati akipambana kumvuta winga kutoka Msumbiji, Luís Jose Miquissone kwa siri ili atue kikosini Jangwani, upande wa pili alikuwa akimpigia hesabu kumbeba winga matata wa TP Mazembe.
Umatemate wa Ghalib inaelezwa umemchanganya winga huyo wa Mazembe, Gnanzou Djeni kutoka Ivory Coast na kutaka atimke DR Congo kwani anaona amekuwa akifanyiwa figisu kucheza kikosi cha kwanza cha timu hiyo, ilhali kuna timu kama Yanga inamtaka akawafanyie mambo.
Inaelezwa kukosa kwake namba kumemfanya Gnanzou aliyekuwa akiichezea San Pedro ya kwao Ivory Coast iliyoshiriki Kombe la Shirikisho msimu wa 2018-2019 kukosa furaha TP Mazembe ya bilionea Moise Katumbi, na anapambana aondoke na akifanikiwa haraka ujue atakuwa hapa nchini.
Gnanzou sio silaha kubwa sana kwa Mazembe, na wanaweza kumuachia kama walivyofanya kwa Deo Kanda waliyemtoa kwa mkopo hata kama watagoma kumvunjia mkataba basi mkopo unaweza kumhusu atue Jangwani.
Ghalib na jeshi lake tayari wameshamchanganya meneja wa mchezaji huyo aliyezungumza na Gnanzou na amekubali kama hesabu zikikaa sawa atakuja nchini.
Walichopanga GSM walio chini ya Ghalib ambao ndio wanaivalisha Yanga na kuijaza jeuri yote ya sasa ni kwamba, mpaka wiki inayoanza leo haijaisha lazima washushe staa mzito atakayewatingisha watani wao, Simba.
Hesabu hizo zinaweza kuangukia kwa Luis endapo watafanikiwa ingawa wanatambua kurejea kwa Simba katika dili hilo kumeongeza ugumu na sasa kama atakosekana huyo, basi aje Gnanzou.
Simba imeingia vitani kuhakikisha wanazuia dili la Luis kutua Yanga, kwani wamepima na kuona kwamba endapo winga huyo atatua upande huo wanaweza kutoka na hali mbaya katika mchezo baina ya timu hizo.
Tayari Wekundu hao wameshamtanguliza mbele Mtendaji wao mkuu, Senzo Mazingisa huko Afrika Kusini kuteta na klabu inayommiliki Luis, Mamelodi Sundown ikimsisititiza hatakiwi kufanya makosa yoyote akiwa huko kwao.
Bilionea huyo wa Yanga amemtanguliza msaidizi wake Mhandisi Hersi Said ambaye mpaka jana alikuwa hajarejea nchini alikokwenda Uganda kumalizana na Ditram Nchimbi, kisha Rwanda kumalizana na kiungo Haruna Niyonzima huku ikikosa kujulikana yuko eneo gani na anafanya ‘vurugu’ gani.
Aidha inaelezwa kwamba kwa sasa mabosi wa kikosi hicho wameamua kufanya mambo kimyakimya wakitaka kuhakikisha wanashtua kabla ya pambano la Simba na Yanga Januari 4, kwa kumleta mtu atakayewatetemesha watani wao.
Klabu hizo mbili kubwa nchini ziko katika harakati nzito za kusuka vikosi vyao, ikielezwa kwamba kila upande haulali ili kuhakikisha mambo yanaenda vizuri.
MWANASPOTI