Inaelezwa uongozi wa Yanga bado haujampa mkataba mshambuliaji raia wa Ivory Coast Yikpe Gnamien ambaye yuko nchini tangu mwishoni mwa wiki iliyopita
Gnamien ametua kumalizana na Yanga akitokea klabu ya Gor Mahia ambayo alivunja mkataba nayo mwezi uliopita baada ya timu hiyo kushindwa kumlipa mishahara
Kamati ya Ufundi ya Yanga imetoa mapendekezo kwa benchi la ufundi kujiridhisha na uwezo wake kabla ya kumpa mkataba
Hata hivyo taarifa zaidi zinabainisha kuwa Gnamien amegoma kufanyiwa majaribio akidai kuwa hayakuwa makubaliano waliyokuwa wameafikiana na viongozi wa Yanga awali
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Ufundi amedokeza kuwa hawataki kufanya makosa kama yaliyojitokeza katika usajili uliopita kupelekea kulazimika kuvunja mikataba ya baadhi ya nyota wa kigeni ambao msaada wao kwa timu umekuwa mdogo
Aidha Afisa Mhamasishaji wa Yanga Antonio Nugaz amesisitiza kuwa ni lazima mchezaji huyo afanyiwe majaribio kama anataka kucheza Yanga
Amesema wamempa masaa 24 akajiunge na timu mkoani Mbeya au abaki jijini Dar es salaam na mpango wa usajili wake kusitishwa