Yanga iko mbioni kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Gor Mahia Gilsein Gnamien Yikpe
Gnamien alitua nchini jana na pengine huenda leo akatambulishwa kuwa mchezaji halali wa Yanga
Gor Mahia ilimsajili Gnamien (23) kutoka klabu ya SC Gagnoa ya Ivory Coast mwezi Julai kuchukua nafasi ya Jacques Tuyisenge aliyesajiliwa na Petro Atletico ya Angola
Hata hivyo mchezaji huyo ameachana na Gor Mahia baada ya kuitumikia kwa miezi minne tu kutokana na ukata uliowakumba mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Kenya
Mapema mwaka huu Gor Mahia ilipoteza udhamini wa kampuni ya Sportpesa ambayo ilifunga biashara zake nchini Kenya baada ya kutokea sintofahamu baina yake na Serikali
Timu hiyo pia iko mbioni kuwapoteza wachezaji wake tegemeo beki Joash Onyango na Kenneth Muguna ambao pia wameomba kuvunja mikataba yao
Katika muda aliyoitumikia Gor Mahia, Yikpe alifunga mabao manne mawili akiyafunga kwenye mchezo wa 'dabi ya mashemeji' kati ya Gor Mahia dhidi ya AFC Leopards, mchezo ambao Gor Mahia ilishinda 4-1

Huko Ivory Coast Yikpe anafahamika zaidi kwa jina la utani la 'Adebayor' kutokana na kuwa na umbo na aina ya uchezaji unaofanana na nyota wa zamani wa Arsenal, Manchester City na Tottenham, Emmanuel Adebayor
Ni mchezaji mwenye uwezo wa kufunga kwa kutumia miguu yote lakini pia akiwa hatari kwa mipira ya vichwa
Unaambiwa Yikpe hana tofauti na Heritier Makambo katika umahiri wa kutumia kichwa chake kufunga mabao
Usajili wake unaifanya safu ya ushambuliaji ya Yanga iwe imekamilika
Kwani anaungana na David Molinga, Ditram Nchimbi naTariq Seif ambao kila mmoja ana umahiri wake katika kucheka na nyavu