Michuano ya kombe la Mapinduzi inatarajiwa kuanza Disemba 31 na kumalizika Januari 13 2020 visiwani Zanzibar
Michuano hiyo itashirikisha timu kutoka Visiwani Zanzibar, Bara na wageni waalikwa kutoka moja ya nchi za ukanda wa Afrika Mashariki
Hata hivyo ushiriki vya vilabu vya Yanga, Simba na Azam Fc huenda ukawa kwenye hatihati kutokana na muingiliano wa ratiba
Kulingana na ratiba ya ligi kuu, mchezo wa watani wa jadi utapigwa Januari 04 2020 na Bodi ya Ligi imesisitiza kuwa mchezo huo utapigwa kama ulivyopangwa
Mwenyekiti wa Bodi, Stephen Mguto amesema wamekuwa wakifanya mabadiliko ya ratiba mara kwa mara kutokana na muingiliano wa kalenda ya michuano mingine, lakini kwa michuano ya kombe la Mapinduzi wametoa mapendekezo ambayo wanaamini yataongeza ufanisi wa michuano hiyo bila ya kuathiri ratiba ya ligi kuu
Mguto amesema wamewashauri ZFA kubadili aina ya mfumo wa mashindano hayo kwa kucheza mechi kwa mtoano na si makundi kama ilivyozoeleka.
Kiongozi huyo alisema kuwa wanataka kuona ratiba ya Ligi Kuu ambayo ilirekebishwa hivi karibuni haipanguliwi tena kutokana na mashindano hayo, kwa sababu tayari waliwapa taarifa ya siku ambazo wanaweza kushirikisha klabu za Tanzania Bara.
"Simba na Yanga wanaweza kwenda kushiriki Kombe la Mapinduzi endapo tu waandaaji watakubaliana na mapendekezo yetu, wakitaka kwenda tofauti nadhani watakuwa hawawahitaji, hii ni kutokana changamoto ya kubadili ratiba iliyotokana na ushiriki wa Taifa Stars na klabu kwenye majukumu ya kimataifa," amesema Mguto.
Aliongeza kuwa mapendekezo ambayo wametoa ni kwa ajili ya kuheshimu umuhimu wa michuano hiyo na kuhakikisha Simba na Yanga zinakwenda Zanzibar kuchuana na hatimaye kuwapa nafasi mashabiki wao wa visiwani kuwaona wachezaji walioko kwenye vikosi hivyo.
Mbali na Simba na Yanga, klabu nyingine ya Tanzania Bara inayotarajiwa kushiriki mashindano hayo ni mabingwa watetezi Azam FC kutoka jijini Dar es Salaam.