Mshambuliaji Luis Miquissone anayecheza kwa mkopo UD Songo akitokea klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, yuko kwenye rada za Yanga inayomuwania kumsajili
Miquissone ndiye aliyeifungia UD Songo bao pekee kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Simba ambao ulipigwa uwanja wa Taifa
Ni bao hilo ambalo liliiondoa Simba hatua ya awali ya michuano hiyo baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1
Timu hizo zilitoka suluhu ya bila kufungana kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Msumbiji
Mshambuliaji huyo yuko mbioni kuvunja mkataba wake na Mamelodi baada ya kukosa nafasi kwenye kikosi cha timu hiyo
Alisajiliwa na Mamelodi kisha akatolewa kwa mkopo UD Songo
Misquissone amekiri kufanya mazungumzo na viongozi watatu wa Yanga, ila akamtaja mmoja ambaye anafahamu vizuri lugha ya Kireno na Kiingereza
"Maongezi yetu yalikuwa mazuri kati ya viongozi hao wote watatu ambao walinipigia simu na hatua ambayo tumefikia wakati huu ni kusubiri kutumiwa tiketi ya kuja huko Tanzania kwani mpaka Passport yangu nimewatumia tayari, " Miquissone amenukuliwa na Mwanaspoti
"Nina mkataba na Mamelodi Sandowns ya Afrika Kusini iliyonirudisha kwa mkopo UD Songo, lakini siku si nyingi naenda kuvunja mkataba wangu na kuwa mchezaji huru ili niweze kusaini popote"
"Nimemaliza majukumu yangu ya UD Songo kwani Ligi ya Msumbuiji imemalizika jana (juzi) Jumatano kwa maana hiyo nipo huru kwenda timu yoyote ili kuzungumza nayo na kama tutakubaliana naweza kusaini hapo"
"Kuhusu mkataba na Mamelodi sina wasiwasi kwangu kwani suala la kuvunja linawezekana kutokana kuna mambo hayakuwa yanakwenda sawa," aliongezea Miquissone.