Suala la changamoto ya ulipaji mishahara halijaanza leo, lakini jambo hili halikusikika miezi miwili mitatu nyuma kwa sababu Yanga ilikuwa na Mwinyi Zahera
Pamoja na kuwa Mkufunzi wa timu, Zahera alikuwa zaidi ya kiongozi Yanga
Wachezaji walimuamini na kumuheshimu kwani alikuwa mzazi kwao, aliwasaidia pale viongozi waliposhindwa kutimiza wajibu wao
Zahera alikuwa akiipenda Yanga kuliko wengi walivyokuwa wakimfikiria
Katumia zaidi ya Tsh Milioni 100 kuihudumia timu wakati yeye akiwa ni kocha tu, ni jambo la kipekee
Zahera aliwasitiri viongozi wa Yanga wasiumbuke. Alilipia gharama za kukodi usafiri, kununulia wachezaji chakula, kulipia mahitaji mengine ya wachezaji wake pale viongozi waliposhindwa
Mcongomani huyu alifikia hatua ya kuwakopesha wachezaji fedha pale walipokosa mishahara yao kwa wakati
Ndio maana wakati wake changamoto pekee iliyokuwa ikizungumza ni suala la matokeo uwanjani
Lakini si kwamba wakati huo wachezaji walikuwa wakilipwa mishahara yao kwa wakati, La hasha..!
Kwani kama mchezaji leo anavunja mkataba baada ya kukosa mishahara kwa miezi mitatu, ina maana alifanya kazi na Zahera kwa miezi miwili bila ya kulipwa mshahara
Ukweli ni kwamba wapo wachezaji ambao walikata tamaa baada ya Zahera kuondolewa kwani hawaoni kama kuna juhudi zinafanyika kuwafanya wafurahie maisha yao ndani ya klabu ya Yanga
Zahera ndiye aliyekuwa akiwasaidia kuendesha maisha yao wakati wakisotea mishahara yao
Sasa leo hayupo nani atawasaidia?
Pengine hili ni funzo kwa viongozi kuwa wakati mwingine hawapaswi kuchukua maamuzi ili mradi tu kuwafurahisha mashabiki
Viongozi waliangalia suala la kumtimua Zahera kijuujuu tu, lakini hawakuangalia kuwa yale aliyokuwa akifanya 'nyuma ya pazia' yangeweza kuiathiri Yanga hasa kama viongozi hawatachukua hatua za kuyafanyia kazi
Uamuzi wa kumuondoa Zahera ulifanywa haraka sana, walipaswa kuhakikisha kuwa wanao uwezo wa kutimiza mahitaji yote ya timu kwa maana ya kumuondolea Zahera majukumu aliyokuwa akifanya nyuma ya pazia
Sasa leo hii ameondoka pengo lake limeonekana haraka tu (athari za kiuchumi) kwa sababu yale aliyokuwa akiyafanya nje ya kazi yake ya ukocha hakuna anayeyafanya ndani ya uongozi wa Yanga
NB : Makala hii imeandikwa na mdau wa Yanga, ni maoni yake binafsi kutokana na kile kinachoendelea Yanga