Unaambiwa tizi wanalopiga wachezaji wa Yanga chini ya kocha Boniface Mkwasa, usipime, inaonesha ni jinsi gani kocha huyo amepania kufanya kweli katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizosalia.
Lengo kubwa la Yanga msimu huu ni kuchukua ubingwa wa ligi hiyo baada ya kuukosa kwa misimu miwili mfululizo.
Baada ya Mkwasa kukabidhiwa kikosi hicho kilichokuwa chini ya Mwinyi Zahera aliyetimuliwa kutokana na matokeo yasiyoridhisha, ameamua kubalisha kila idara.
Mkwasa amebadilisha kikosi hicho kuanzia program ya mazoezi hadi nafasi za wachezaji tofauti na walivyokuwa wakitumika kwa Zahera.
Picha ya kikosi cha Mkwasa ilianza kuonekana katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Coastal Union, Yanga wakiibuka na ushindi wa mabao 3-1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, wapenzi wa Yanga walishuhudia ile radha halisi ya Papy Tshishimbi, aliyecheza katika eneo lake la kiungo namba sita tofauti na alivyokuwa akichezeshwa huko nyuma
Pia Ally Mtoni sasa hivi anacheza nafasi ya beki wa kati, badala ya namba tatu aliyokuwa anachezeshwa na ameonekana kuwa huru zaidi

Akizungumzia mabadiliko hayo, Mkwasa alisema anachotaka ni kuingia na mfumo wake utakaomuwezesha kupata matokeo na wachezaji kuwa fiti zaidi.
"Kwa muda huu niliopewa, nataka kutumia falsafa yangu kulingana na wachezaji waliopo, hakuna mchezaji mbaya katika kikosi cha Yanga kwa sasa, wote wako vizuri," alisema
Leo Yanga imeendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, Dar es Salaam, kujiandaa na mechi ya ligi kuu dhidi ya JKT Tanzania ambayo itapigwa keshokutwa Ijumaa, uwanja wa Uhuru
Mchezo huo umerudishwa nyuma kwa siku moja kwani awali ulipangwa kupigwa Jumamosi, Novemba 23