Kuelekea dirisha dogo la usajili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, amesema atatoa tathimini ya wachezaji wapya anaowahitaji ikiwa ni pamoja na wakukatwa ili kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo mapema wiki ijayo
Mkwasa anayekaimu nafasi ya Kocha Mkuu baada ya Yanga kuachana na Mwinyi Zahera, amesema atatoa tathimini ya wachezaji wanaopaswa kuongezwa na kuachwa kwenye kikosi hicho kwa ajili ya kuanza mchakato mpya wa kusajili wachezaji atakaowahitaji.
Mkwasa alisema baada ya kukutana na Kamati ya Ufundi, watashauriana na kufanya uamuzi wa pamoja kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho wa kikosi wanachokihitaji kuendelea nacho katika vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya Kombe la FA nchini.
"Kwa muda ambao nimekaa na timu, tayari nimeshaanza kuifanyia kazi ripoti ya kiufundi, hadi wiki ijayo nitakuwa nimekamilisha ripoti yangu ya kiufundi kuhusu usajili wa dirisha dogo, ila nitawasiliana na Kamati ya Ufundi kwa ajili ya ushauri zaidi," Mkwasa amenukuliwa na gazeti la Nipashe
Kocha huyo aliongeza kuwa anaamini baada ya usajili huo mdogo kufanyika, kikosi cha Yanga kitarejea kwenye upinzani
"Bado ligi haijakolea, mechi tulizocheza ni chache na kama tutatulia, lolote linaweza kutokea kwenye vita ya ubingwa," alisema