Baada ya misukosuko ya hapa na pale wiki hii, maisha lazima yaendelee..! Ndivyo unavyoweza kusema wakati mabingwa wa kihistoria Yanga wakitarajiwa kushuka kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara kuikabili Ndanda Fc katika mchezo wa Ligi Kuu
Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga Charles Mkwasa 'Master' pamoja na kikosi chake leo watakuwa na kazi moja tu, kusaka alama tatu ugenini
Ni mchezo ambao matokeo ya ushindi ni muhimu sana kwa Yanga kwani ni ushindi pekee ambao utawaunganisha Wanayanga kuepuka mgogoro baada ya mabadiliko ya benchi la ufundi
Pamoja na kuwakosa nyota wake nane, Mkwasa amesema kikosi chake kiko imara, matumaini ya kuibuka na ushindi leo ni makubwa
Yanga ilianza ligi kwa kusuasua lakini mpaka sasa kama itashinda mechi zake zote za viporo, itaweza kuwafikia vinara wa ligi hiyo Simba
Jana Simba ililazimishwa suluhu ya bila kufungana na Tanzania Prisons hivyo imepoteza jumla ya alama tano kama ilivyo kwa Yanga
Mashabiki wa Yanga mkoani Mtwara wametakiwa kujitokeza kwa wingi dimba la Nangwanda kuiunga mkono timu yao ili iweze kuibuka na ushindi