Wakati Mwinyi Zahera akitupiwa virago Yanga jana, mchezaji wa timu hiyo, Balama Mapinduzi amesema imekuwa kama sapraizi kwao.
Yanga imetangaza kuachana na kocha huyo Mkongo ikiwa ni siku chache tangu walipoondoshwa katika mashindano ya kimataifa.
"Ni kama sapraizi kwetu, tulikuwa naye mazoezi ya leo (jana) asubuhi wala hakuonyesha kama kuna taarifa yoyote juu ya kuondoka," Balama amenukuliwa na Mwanaspoti
"Amesimamia mazoezi mwanzo mwisho, akatupa na programu ya kesho (leo), hii taarifa ya kwamba ametimuliwa ni sapraizi kwangu"
Balama ameungana na Feisal Salim (Fei Toto) ambaye pia amesema kuondoka kwa Zahera ni jambo geni kwake.
"Mbona tulikuwa naye mazoezi na hakuonyesha dalili yoyote wala kutuaga kwamba anaondoka, sitaki kuamini kama ni kweli japo hiyo ni kawaida kwa makocha," alisema Fei Toto
Baada ya kocha huyo na benchi lote la ufundi kuvunjwa, kwa sasa Yanga iko chini ya kocha wa muda Charles Mkwasa ambapo Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla amesema ataiongoza timu katika kipindi cha mpito cha wiki mbili
Timu imeelekea mkoani Mtwara leo tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ndanda Fc ambao utapigwa keshokutwa Ijumaa kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona