Msimu uliopita Yanga ilikuwa na wakati mgumu sana, kama sio Mwinyi Zahera pengine mambo ya kushangaza yangeshuhudiwa
Licha kukutana na mazingira magumu, Zahera alijitolea kwa moyo wote kuipigania Yanga
Kuna wakati machozi yalimtoka pale timu yake ilipofanyiwa maonevu na waamuzi
Alibuni njia mbalimbali za kuiongezea timu mapato lengo likiwa kujenga timu imara itakayoweza kutoa ushindani wa kweli
Lakini kumbe hakufahamu jitihada hizo lilikuwa kaburi lake
Ni usajili wake aliofanya kutokana na fedha hizo umekuwa sababu ya yeye kutimuliwa ingawa kimsingi uamuzi huo umechukuliwa kwa 'pupa'
Ametoa sababu nyingi kwa timu kutofanya vizuri, nyingi zilikuwa na mashiko lakini pengine alikosea wakati wa kuzitoa
Ameondoshwa akiwa amepoteza mchezo mmoja tu kwenye ligi, kashinda miwili na sare moja
Pamoja na kuchelewa kupata taarifa, aliiwezesha Yanga kuvuka raundi ya kwanza ya michuano ya ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya timu ya Township Rollers
Kuelekea mchezo wa Rollers wanayanga wengi walikuwa wamekata tamaa kwa sababu kwanza timu haikuwa na maandalizi mazuri
Lakini pia Rollers wanaifahamu, ilikuja Tanzania msimu mmoja nyuma na kuondoka na ushindi uwanja wa Taifa
Timu imeingia raundi ya kwanza, ikaondoshwa na Zesco United kwa bahati mbaya kwa bao la kujifunga la Makame
Pamoja na kulaumiwa kuwa timu yake haichezi vizuri, lakini Zahera alikuwa na mbinu za kupata matokeo katika michezo migumu
Pyramids Fc hakikuwa kipimo sahihi kwa Yanga kila mmoja anafahamu. Na bila shaka uongozi wa Yanga umemuondoa Zahera kutokana na sababu nyingine na sio kufungwa na Pyramids Fc
Kwani hakuna namna ambayo Yanga inaweza kujilinganisha na Pyramids Fc, huu utabaki kuwa ukweli
Kazi ya ukocha wa mpira wa miguu ni ngumu sana, kwani unaajiriwa ili ufukuzwe
Ukisaini mkataba leo unaanza kuhesabu siku kuelekea siku yako ya kufukuzwa
Umefika wakati uongozi wa Yanga umeona unahitaji kufanya mabadiliko benchi lake la ufundi, hivyo uamuzi huo uheshimiwe
Lakini kwa ambayo Zahera amaeifanyia Yanga, hakika sitathubutu kumlaumu, nitamtakia kila la kheri huko aendako..