Mshambuliaji wa KCCA ya Uganda, Allan Okello, ameitaka Yanga kumpa muda Juma Balinya ili waweze kufaidi ubora wake .
Balinya aliyesajiwa na Yanga katika dirisha kubwa la usajili lililofungwa Julai mwaka huu, akitokea Polisi ya Uganda hajaonyesha ubora wake.
Mshambuliaji huyo alimaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu Uganda, akiwa mfungaji bora aliyefikisha mabao 19.
Okello amesema anamfahamu Balinya ni mchezaji mzuri ambaye alikuwa akiwapa changamoto nchini Uganda
Mkali huyo wa kuzifumania nyavu amesisitiza kuwa Balinya ni moto wa kuotea mbali japo ameonekana kutokuwa vizuri akiwa ndani ya kikosi cha Yanga.
Anaamini mshambuliaji huyo wa Yanga bado hajaizoea ligi ya Tanzania baada ya kubadilisha mazingira ambayo inaonekana ni changamoto kwake.
“Balinya namfahamu sijacheza naye klabu moja lakini ligi yetu ni moja hakuna ambaye hamjui kutokana na ubora alionao.
“Nadhani mabadiliko ya hali ya hewa ni changamoto kwake ametoka Uganda amekuja kucheza Tanzania, akipewa muda wa kutosha watamwelewa ni mchezaji wa aina gani,” alisema Okello.