Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema wanakwenda Misri kusaka matokeo ya ushindi na si vinginevyo
Akizungumza jana mda mfupi kabla ya kuianza safari ya Misri kuifuata Pyramids Fc kwa ajili ya mchezo wa marudiano ambao utapigwa keshokutwa Novemba 03 kwenye uwanja wa June 30, Zahera alisema kama wachezaji watafuata maelekezo waliyopeana mazoezi, uwezo wa kufunga zaidi ya mabao mawili ugenini wanao
"Ukiangalia mchezo wa kwanza tulifungwa kwa bahati mbaya. Bao la pili walilotufunga lilitokana na sisi wenyewe kukosa umakini," alisema
"Lakini pia tuliweza kuwafunga bao ambapo katika dakika 15 za mwisho tulifanya mashambulizi mengi langoni kwao"
"Mbinu tuliyotumia kwenye mchezo wa kwanza haikufanikiwa kwa kuwa wapinzani wetu walibaini mapema mpango wetu, mchezo wa marudiano tutabadilika"
"Tunahitaji kufunga mabao sio chini ya mawili, tutatumia mbinu ya kushambulia zaidi kama tulivyofanya kipindi cha pili"
Pyramids Fc hawatishi Misri - Mwakalebela
Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela alitangulia nchini Misri kuandaa mapokezi ya timu
Mwakalebela amesema nchini Misri Pyramids Fc inachukuliwa kama timu ya kawaida, jambo ambalo limewapa moyo kuwa wanaweza kupindua meza
"Hapa Misri wanaizungumzia Pyramids Fc kama timu ya kawaida tu. Hili linatupa moyo tukipambana tunaweza kuondoka na ushindi," amesema
Yanga inahitaji kushinda 2-0 kuweza kutinga makundi, ushindi wa 2-1 utaupeleka mchezo huo kwenye changamoto ya mikwaju ya penati
Lakini kama Yanga itashinda kuanzia mabao matatu, pia itafuzu makundi moja kwa moja