Msafara wa wachezaji 20 wa Yanga wanatarajiwa kuondoka kesho Alhamisi kuelekea nchini Misri tayari kwa mchezo wa marudiano kombe la Shirikisho dhidi ya Pyramids Fc
Mchezo huo utapigwa siku ya Jumapili, Novemba 03 katika uwanja wa 30 June ambao unachukua mashabiki takribani 30,000
Uongozi wa klabu ya Yanga umesema wanakwenda Misri kushindana, wameuchukulia mchezo huo kwa uzito kwani bado wana nafasi ya kusonga mbele
Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema wanafahamu wana kazi kubwa ya kufanya huko Misri, wamejipanga kuifanya
"Sisi falsafa yetu ni kupindua meza kibabe, hata kama meza ni ya chuma, tutaipindua hivyohivyo," ametamba Mwakalebela
Kiongozi huyo anatarajiwa kuongoza msafara huo unaokwenda Misri
Yanga ilirejea kutoka jijini Mwanza juzi na moja kwa moja kuingia kambini kujiandaa na mchezo huo ambao wanahitaji ushindi wa kuanzia mabao mawili