Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesisitiza kuwa hapaswi kulaumiwa baada ya kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Pyramids Fc mchezo wa kwanza wa kombe la Shirikisho barani Afrika
Akihojiwa na redio moja mapema leo, Zahera alisema kwa uzoefu alionao wa soka la Afrika, anafahamu ni kawaida kwa mashabiki kukasirika pale timu zao zinapokuwa hazifanyi vizuri
Lakini amesisitiza timu yake haikuwa katika ubora sawa na wapinzani wao Pyramids Fc
Zahera amebainisha kuwa Yanga aliyoiunda haikuwa kwa ajili ya michuano ya Kimataifa, kwani nafasi hii waliipata wakati wakiwa tayari wameshamaliza usajili wao
"Mashabiki walikuwa wanangoja tuifunge Pyramids Fc, niambie mchezaji mmoja wangu ambaye anaweza kuchezea Pyramids Fc, yupo?," alihoji Zahera
"Wakati tunafanya usajili, tulisajili wachezaji kwa ajili ya Ligi na sio michuano hii"
"Mimi waliniambia tutashiriki Ligi ya Mabingwa wakati nikiwa Congo na timu ya Taifa kwa ajili ya AFCON"
"Waniulize maswali kama sitafanya vizuri kwenye ligi. Lakini hatukuwa tumeandaa timu kwa ajili ya michuano hii"
"Hatuwezi kujilinganisha na Pyramids, TP Mazembe, Al Ahly na timu nyingine ambazo tangu mapema walifahamu watashiriki Ligi ya mabingwa au kombe la Shirikisho hivyo wakafanya maandalizi mapema"