Kocha Msaidizi wa Yanga Noel Mwandila amesema kipigo cha mabao 2-1 walichopata kutoka kwa Pyramids Fc kilitokana na makosa waliyofanya kwenye mchezo huo uliopigwa uwanja wa CCM Kirumba
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo, Mwandila alisema mpira wa miguu ni mchezo wa makosa, Pyramids imeiadhibuYanga baada ya kufanya makosa
"Ulikuwa mchezo mgumu, nafikiri kwenye kipindi cha kwanza Pyramids walikuja na mbinu ya kupeleka mipira mbele, wakiwa bora kwenye matukio muhimu ya mchezo"
"Katika dakika 10 za kwanza walituweka kwenye wakati mgumu, walituweka katika presha kubwa na tulishindwa kucheza kutokea nyuma"
"Baada ya muda tulikaa sawa, lakini nadhani ulikuwa mchezo wa vipindi viwili, kipindi cha kwanza hatukufanya vizuri sana kutokana na mbinu waliyotumia Pyramids"
"Tulifahamu katika michezo ya aina hii kama ukifanya makosa utaadhibiwa na kwa bahati mbaya tuliruhusu bao wakati mchezo ukielekea mapumziko"
"Kipindi cha pili tulijaribu kurejea mchezo lakini kwa bahati mbaya tena tukafanya makosa ya kitoto, kukosekana kwa umakini kukapelekea turuhusu bao la pili"
Aidha Mwandila ametetea mfumo wa mshambuliaji mmoja waliotumia kwenye kipindi cha kwanza ambao ulionekana kuipa changamoto Yanga
"Mara nyingi tunacheza na mshambuliaji mmoja, muhimu ni vile wachezaji wanavyotimiza majukumu yao"
"Lakini kama una wachezaji hawawezi kutekeleza ipasavyo kile wanachopaswa kufanya wanapokuwa na mpira au bila mpira inakuwa ngumu"
"Siku ya leo kilichotupa wakati mgumu ni mbinu waliyotumia Pyramids Fc hasa kwenye kipindi cha kwanza"
"Unaweza kucheza na mshambuliaji mmoja, wawili au watatu haijalishi, muhimu ni vile jinsi wanavyocheza kulingana na nini wanapaswa kufanya"