Timu haikucheza vizuri kipindi cha kwanza, wachezaji wa Yanga walionekana kutokujiamini huku wakishindwa kuutumia uwanja wa CCM Kirumba kana kwamba ilikuwa mara ya kwanza kucheza hapo
Pyramids Fc walijiamini huku wakionekana kuzoea kwa haraka mazingira ya uwanja
Kwenye kipindi cha kwanza kocha Mwinyi Zahera alifeli kimbinu, mfumo alioutumia uliwarahisishia kazi Pyramids Fc
Haikuwa sahihi kwa Yanga kutumia mshambuliaji mmoja katika mchezo huu ambao timu iko nyumbani
Pia kwa kuwa hali ya uwanja wa CCM Kirumba hairuhusu timu kucheza pasi za chinichini, angalau timu ingekuwa na washambuliaji wawili mbele kuwapa changamoto walinzi wa Pyramids
Mipira mirefu haikuwa na faida kwa Yanga kwa sababu mabeki wa Pyramids ni warefu. Matokeo yake mipira yote ya juu walikuwa wakicheza wao
Kipindi cha pili Yanga ilibadilika kwa kuweka mpira chini, lakini bado tatizo likabaki kwenye safu ya ushambuliaji kwani muda mwingi Sadney alikuwa akibaki peke yake
Wakati wa kushambulia wachezaji wa Yanga walichelewa kuongeza namba langoni kwa Pyramids hivyo kuwafanya walinzi wao wawe huru
Hata hivyo baada ya kuwaingiza Balinya na baadae Sibomana Yanga ilianza kulishambulia lango la Pyramids
Walinzi wa timu hiyo wakafanya makosa ambayo hata hivyo Yanga haikuweza kuyatumia kupitia mipira ya adhabu
Balinya ana tatizo gani?
Kwanza hakuwemo kwenye kikosi kilichotolewa awali lakini baadae akaongezwa, ilidhaniwa ni majeruhi
Lakini alipoingia, kwa dakika chache alizocheza aliongeza kitu
Bado wengi wamekuwa na maswali kwa nini kocha Mwinyi Zahera hamtumii mshambuliaji huyu aliyekuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Uganda msimu uliopita
Lakini mwisho wa siku ni kocha anayefahamu ni mchezaji yupi amtumie ili kuweza kupata matokeo
Ngasa alifanya kosa la 'kitoto'
Kwa uzoefu alionao Mrisho Ngasa, kosa alilofanya ambalo lilipelekea Pyramids kufunga bao la pili, hatalisahau
Ngasa alipaswa kucheza na mwamuzi au ahakikishe mpira umetoka kabisa na sio kuuacha utoke wenyewe
Pengine kutokuwa mlinzi kumechangia kwani mara nyingi mabeki wanahakikisha wanaulinda mpira hadi pale unapotoka
Nini kifanyike Misri
Yanga haina cha kupoteza mchezo wa ugenini kwa kuwa tayari imefungwa nyumbani
Timu inapaswa kwenda na mbinu ya kushambulia, huku wakiwa na uwiano mzuri katika ulinzi
Pamoja na ubora wao, Pyramids Fc sio timu ya kutisha. Ukiwashambulia una nafasi ya kuwafunga
Wameruhusu mabao kwenye uwanja wao wa nyumbani kwenye kila mchezo waliocheza kwenye michuano hii
Yanga inahitaji kufunga mabao mawili au zaidi ugenini, inawezekana