Viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) pamoja na wale wa Yanga, wameungana kuhakikisha Yanga inashinda mchezo dhidi ya Pyramids Fc keshokutwa
Rais wa TFF Wallace Karia amesema shirikisho limetuma viongozi wake Mwanza wafanye kazi bega kwa bega na wenzao wa Yanga
Karia amesema Yanga ndio muwakilishi pekee wa Tanzania Bara katika michuano ya vilabu barani Afrika baada ya KMC, Simba na Azam Fc kutolewa
Amesema mabingwa hao wa kihistoria wana jukumu la kulinda nafasi nne ambazo Tanzania ilizipata baada ya mafanikio ya Simba msimu uliopita
Kama Yanga itafanikiwa kutinga hatua ya makundi, itaongeza alama ambazo pia zitaongezeka mara dufu kama watafanya vizuri kwenye makundi
"Lazima tupambane Yanga iingie makundi, katika nchi ambazo zinagombea pointi hizo, washindani wetu pia wamo kama Gor Mahia ambaye naye hajatolewa kimataifa, lazima tupambane ili pointi zetu ziongezeke na tuendelee kuwa na timu nne kimataifa msimu ujao," amesema
"Tulikaa na viongozi wa Yanga awali na baada ya kuamua mechi yao ikachezwe Mwanza, tulishauriana na bado tunaendelea kushirikiana kwa hali na mali, hii ni mechi ya Watanzania hivyo hatuna budi kuhakikisha tunashinda kama Taifa"