Uongozi wa Yanga umewataka mashabiki wa timu hiyo kutovamia uwanja baada ya mchezo wao dhidi ya Pyramids katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Mashabiki wa Yanga katika jiji la Mwanza wamekuwa na tabia ya kuvamia uwanja kila mechi inapomalizika hasa timu yao inapokuwa imeshinda.
Akizungumza jijini Mwanza, leo Ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amewataka mashabiki kutofanya kitendo hicho katika mchezo wao wa Jumapili dhidi ya Pyramids.
Bumbuli amesema hata kama wakipata ushindi mnono ambao utawapa furaha ya kupitiliza mashabiki wao, lakini wasiingie uwanjani kushangilia kwani watahesabika na CAF kuwa walianzisha vurugu ambazo kisheria zinaweza kuwapotezea nafasi yao.
A,esema mashabiki wanapaswa kuwa watulivu, lakini wakiishangilia timu yao ameongeza usalama wa wapinzani wao upo chini yao hivyo wanapaswa kushirikiana kudumisha amani ili kuepuka migogoro.
Hata hivyo Bumbuli alisema mashabiki wenye tabia ya kuruka ukuta kabla ya mchezo na baada kutokana na sababu zozote zile, wasijaribu kufanya hivyo kwani ulinzi utakuwa wa maana kwenye pambano hilo.
"Ulinzi utakuwa wa uhakika, nawaomba mashabiki wawe watulivu lakini waishangilie timu yao, tafadhari suala la kuingia uwanjani baada ya mechi litatuharibia, wasifanye hivyo hata kidogo" alisema Bumbuli.