Afisa Uhamasishaji na Msemaji wa klabu ya Yanga Antonio Nugaz amesema mpango wa kuupeleka jijini Mwanza mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Pyramids Fc haukutokea kwa bahati mbaya
Nugaz amesema uongozi wa timu hiyo ulikuwa na mpango wa kucheza mechi zake katika mikoa tofauti kama wangetinga makundi ligi ya mabingwa
"Tulipanga kucheza Zanzibar, Dar na Mwanza kama tungetinga makundi ligi ya mabingwa," Nugaz aliiambia Azam TV
"Hivyo hatukurupuka kupeleka mchezo wetu dhidi ya Pyramids jijini Mwanza"
Aidha Nugaz amesema wamejipanga kufanya shughuli mbalimbali za kijamii jijini Mwanza
Amesema Yanga itatoa misaada mbalimbali kwa wahitaji kama sehemu ya kurejesha kwa jamii
Miongoni mwa misaada hiyo wamepanga kuchimba kisima kwa wananchi wenye uhaba wa huduma ya maji