Kikosi cha mabingwa wa kihistoria Tanzania Yanga leo kinashuka uwanja wa Uhuru kuikabili Coastal Union katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara
Yanga imekusanya alama moja tu kutoka michezo miwili, leo wanahitaji ushindi
Juzi walipata alama hiyo baada ya kuambulia sare ya mabao 3-3 dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo ambao walikuwa na matumaini ya kushinda
Mazingira hayo yanaufanya mchezo wa leo kuwa kama fainali kwao
Matokeo tofauti na ushindi yatazidi kuwaweka pabaya mapema tu katika mbio za kuwania ubingwa walioupoteza kwa watani zao misimu miwili sasa
Yanga wataingia kwenye mchezo huo utakaopigwa uwanja wa Uhuru wakiwa na lengo moja tu, kuondoka na alama zote tatu
Ni mchezo ambao kama Yanga watauanza vizuri, unaweza kushuhudia idadi kubwa ya mabao
Walikuwa na changamoto ya kufunga mabao, lakini sasa tatizo hilo linaonekana kupata suluhu kutokana na uwepo wa Mcongoman David Molinga
Ari ya wachezaji iko juu, huu ni mchezo ambao wana kila sababu ya kushinda
Hata hivyo pamoja na kuhitaji ushindi, ni mchezo ambao safu ya ulinzi inapaswa kuongeza umakini
Waliruhusu mabao matatu kwenye mchezo uliopita, hawapaswi kufanya makosa yaleyale ambayo yanaweza kuwaweka kwenye wakati mgumu