Afisa Uhamasishaji wa Yanga Antonio Nugaz amesema wamekubali matokeo ya sare ya mabao 3-3 dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Uhuru jana
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo, Nugaz amesema ulikuwa ni mchezo wenye ushindani huku Polisi Tanzania wakichagizwa na uwepo wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Simon Sirro
"Ulikuwa ni mchezo wenye ushindani mkubwa. Hatukucheza vizuri sana lakini naamini tutakaa sawa. Timu yetu ina wachezaji 18 wapya, inahitaji muda zaidi wa wachezaji kuzoeana"
"Hata hivyo tungemfunga vipi Polisi mbele ya IGP?," alihoji Nugaz
Akizungumzia mabadiliko ya mara kwa mara ya kikosi cha kwanza yanayofanywa na kocha Mwinyi Zahera, Nugaz amesema bado hajapata kikosi cha kwanza
"Kocha bado anatafuta kikosi chake cha kwanza, anawapa nafasi wachezaji wote ili kufahamu namna wanavyoweza kwendana na mfumo wake"
"Leo amemuanzisha Juma Abdul, umeona tofauti"
Katika hatua nyingine Nugaz amewataka waandishi wa habari kuihoji TFF juu ya adhabu ya kuvaa 'pensi' aliyopewa kocha Zahera licha ya makocha wengine kuendelea kutumia vazi hilo
"Sisi viongozi bado tunajiuliza tulipokosea wapi, lakini nyinyi waandishi kawaulizeni TFF mbona adhabu hii alipewa kocha mmoja tu wakati upo ushahidi wa makocha wengine kuvaa kama yeye?"
Zahera aliushuhudia mchezo wa timu yake jana akiwa jukwaani huku akiwa 'amepigilia' pensi kama ilivyo kawaida yake
Anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu