Kocha Mkuu wa Zesco United George Lwandamina ameeleza kushangazwa na uwezo ulioonyeshwa na wachezaji wa Yanga kwenye mchezo baina ya timu hizo uliopigwa uwanja wa Levy Mwanawasa jana nchini Zambia na Zesco kuibuka na ushindi wa mabao 2-1
Akizungumza baada ya mchezo huo, Lwandamina alisema Yanga iliweza kutawala safu ya kiungo kwenye kipindi chote cha kwanza na kuwapa wakati mgumu vijana wake ambao walilazimika kutumia mipira mirefu
Alisema ameona timu imesheheni wachezaji wengi wapya, anaamini baada ya muda Yanga itakuwa tishio ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa jangwa la sahara
Aidha kocha huyo mpole amesema bado anaikumbuka Yanga, anaamini siku moja anaweza kurejea Tanzania katika klabu hiyo
"Ilikuwa zaidi ya vita ambapo timu mbili imara zilikutana, Yanga SC ni timu ina wachezaji wote wapya ila nakuhakikishia wakikaa pamoja zaidi itakuja kuwa timu tishio zaidi kwa vilabu vyote kusini mwa Afrika," alisema
"Hatukutegemea kupata upinzani wa namna hii hasa kipindi cha kwanza ambapo walikiteka kiungo 100"
"Yanga ni timu yangu ni familia yangu ila nimetimiza kazi yangu hapa Zesco, najua kuna watu bado wananikumbuka na kunihitaji muda ukiwa sahihi ntarudi tena nyumbani"
Lwandamina aliondoka Yanga baada ya changamoto za kiuchumi 'kushika hatamu'
Wakati yuko Yanga Mzambia huyo alikuwa akipendwa sana na wachezaji pamoja na viongozi kutokana na tabia yake ya ukarimu
Kuna wakati alikataa kupokea mshahara wake kabla ya wachezaji kulipwa madai yao
Pamoja na kuwa na madeni kwa uongozi wa Yanga, Lwandamina aliondoka kwa roho safi
Mzambia huyo bado anaamini hakukamilisha kile alichokuwa amekifuata Yanga