Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera amedhihirisha kuwa yeye ni zaidi ya kocha hasa linapokuja suala la timu kupata matokeo
Pamoja na kuiandaa timu kimbinu, Zahera ni bingwa wa kuwaandaa wachezaji wake kisaikolojia kabla ya mchezo
Wengi wanakumbuka msimu uliopita, pamoja na kuwa kikosi cha kawaida, Yanga ilikuwa timu isiyotabirika kwani ilipata matokeo kila mara iliposhuka dimbani ingawa wengi hawakuipa nafasi ya kufanya vizuri
Leo ana kazi muhimu ya kukiongoza kikosi chake kuiangusha Zesco United katika uwanja wao wa nyumbani
Michezo ya aina hii ndio ambayo utauona umahiri wa kocha Zahera
Ni kocha anayejiamini na huja na mbinu ambazo mara nyingi huisaidia timu yake kufanya vizuri
Zahera anafahamu umuhimu wa kuipeleka Yanga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa
Pamoja na timu kunufaika kiuchumi, kwa Yanga kutinga hatua ya makundi ni kukamilika kwa moja ya ahadi alizoweka Zahera kuifanya Yanga kuwa moja ya timu bora barani Afrika
Wakati Simba msimu uliopita walitamba kuingia robo fainali, kama Yanga itavuka hatua hii leo, itafanya vizuri zaidi kwenye makundi
Pamoja na changamoto ya uhaba wa mabao, mpaka sasa Yanga imekuwa na kampeni nzuri kwenye michuano hiyo ikiwa haijafungwa katika michezo yote mitatu waliyocheza mpaka sasa
Yanga imeonyesha kuwa imara inapocheza ugenini ukilinganisha na watani zao Simba ambao msimu uliopita ulihitaji kunywa panadol kuweza kutazama michezo yao ya ugenini
Leo ni siku muhimu kwa kocha Zahera ambaye aliwahi kufundisha soka nchini Zambia kwa muda mfupi kabla ya kujiunga na Yanga
Katika benchi atasaidiwa na Noel Mwandila ambaye ni Mzambia, aliwahi kutamba kwenye soka la nchi hiyo
Alifanya kazi kwa muda mrefu na kocha George Lwandamina ambaye leo hii ataiongoza Zesco United
Hata ujio wake Yanga ulifanikishwa na Lwandamina lakini baadae akagoma kurudi Zambia akitaka kutengeneza CV yake zaidi akiwa na Yanga
Hakuna shaka mafanikio ya Yanga leo yatachangiwa kwa kiasi kikubwa na Mwandila ambaye anamfahamu vizuri Lwandamina, lakini pia analifahamu vizuri sana soka la Zambia