Kwa shabiki ambaye anaifuatilia Yanga tangu baada ya mchezo dhidi ya Kariobang Sharks, atakubaliana nami timu imekuwa ikionyesha mabadiliko kila mchezo
Sare ya bao 1-1 dhidi ya ZESCO United jana imewaumiza sana mashabiki kwa kuwa wengi walitegemea kutoka na ushindi
Lakini ndio matokeo ya mpira wa miguu yalivyo, wakati mwingine hayawi ya kufurahisha
Pamoja na kuimarika kwa kikosi cha Yanga, inashangaza kuona baadhi ya mashabiki wanamshushia lawama kocha Mwinyi Zahera kuwa hafai
Sawa, Zahera anaweza kuwajibika kwa kuwa ndiye kocha Mkuu lakini ukiangalia upande wa pili wachezaji wanawajibika kwa nafasi zao?
Hivi unawezaje kumlaumu kocha kuwa timu haishindi wakati ni wachezaji wanaoshindwa kufunga mabao?
Tatizo lingekuwa kubwa kama timu haitengenezi nafasi lakini sivyo
Mchezo dhidi ya ZESCO jana, ukiachilia mbali bao la mkwaju wa penati lililofungwa na Sibomana, Yanga ilitengeneza nafasi sio chini ya tano
Moja ya nafasi muhimu ilipotezwa na nahodha Papy Tshishimbi kwenye kipindi cha pili akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga akatoa mpira nje
Lakini mshambuliaji Sadney Khoutage naye alipoteza nafasi kadhaa pamoja na kusababisha mkwaju wa penati
Pengine kama nafasi hizo zingetumika leo baadhi ya mashabiki wasingemshushia lawama Zahera
Leo hii Zahera analaumiwa kwa kuwa safu yake ya ushambuliaji ni 'butu' lakini timu imesajili wachezaji ambao takwimu zao huko walikotoka walikuwa wakifanya vizuri
Sasa hapa pengine badala ya kumlaumu kocha peke yake, ni vyema kuwauliza wachezaji ambao hawafanyi vizuri kulikoni?
Mwanzoni kabisa Zahera aliwatumia washambuliaji Sibomana, Sadney na Balinya lakini hakukuwa na mafanikio
Mchezo wa jana amelazimika kumuanzisha Tshishimbi namba 10 akicheza nyuma ya Sadney uamuzi huo ni katika jitihada za kutengeneza 'combination' inayoweza kuzalisha mabao
Ni bahati mbaya David Molinga hakuwa na leseni ya kumruhusu kushiriki hatua hii, lakini kama angekuwepo pengine safu ya ushambuliaji ingekuwa tofauti jana
cutJambo la muhimu hapa ni mashabiki kuendelea kuwa wavumilivu wakati kocha akiendelea kufanyia kazi changamoto ya washambuliaji wake
Kumlaumu kwamba alisajili wachezaji wabovu sio sawa kwa kuwa wachezaji hao huko walikotoka walikuwa wakifanya vizuri
Ni kawaida mchezaji anaweza kufanya vizuri timu A lakini akashindwa kufanya vizuri timu B
Mifano iko mingi hapa Tanzania, Afrika na hata ligi za ulaya ambazo wengi tunazifuatilia
Ramadel Falcao alikuwa mwiba alipokuwa Atletico Madrid na AS Monaco lakini alipotua Manchester United mambo hayakumnyookea, pengine hakupewa muda
Angel Di Maria, Mephis Depay nao waliwahi kukumbana na changamoto hiyo Manchester United, lakini Di Maria alipotua PSG mambo yakamnyookea wakati Depay anatamba Lyon na timu ya Taifa ya Uholanzi
Romelu Lukaku, Alexis Sanchez nao wako katika mkondo huo
Tumemuona Eden Hazard aliyetoka Chelsea karibuni sio yule ambaye yuko Real Madrid leo. Lakini wenzetu ni wavumilivu watampa muda ili athibitishe ubora wake
Lakini pia hapahapa Yanga kuna wachezaji walianza kwa kusuasua na kuitwa majina yote yasiyofaa lakini baadae wakawa tegemeo
Waangalie Saimon Msuva na Obrey Chirwa maisha yao walipoanza kuitumikia Yanga
Yanga hii ni mpya zaidi ya asilimia 90 ya wachezaji wa kikosi cha kwanza ni wapya. pengine bado muda unahitajika kuwaweka sawa
Wakati huu hata akiletwa Pep Guardiola Yanga hakutakuwa na muujiza, kwani wachezaji atakaowatumia ni hawahawa