Yanga imerejea jijini Dar es salaam Alfajiri ya leo ikitokea Mwanza ilikokuwa imeweka kambi kujiandaa na mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya ZESCO United
Mabingwa hao wa kihistoria leo wanamalizia maandalizi yao kwenye uwanja wa Taifa kuelekea mchezo huo ambao utapigwa Jumamosi
Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema alitumia kambi ya mkoani Mwanza kuwasoma wapinzani wake, na mpaka sasa tayari wanafahamu jinsi watakavyowakabili
Amesema walipata nafasi ya kuangalia michezo kadhaa ya ZESCO United ambayo imewasaidia kubaini uimara na udhaifu wa timu hiyo
"Hatuna wasiwasi, tumefanya maandalizi mazuri, wachezaji wangu wanajua nini tunapaswa kufanya Jumamosi ili tuweze kushinda," amesema
"Tukiwa Mwanza tulipata muda mzuri wa kujiandaa, tumewasoma wapinzani wetu, nadhani tuna nafasi ya kufanya vizuri"
"Tunafahamu tunapaswa kushinda mchezo huu wa nyumbani kuwa na nafasi ya kuingia hatua ya makundi"
Ikiwa Mwanza Yanga ilicheza michezo miwili ya kirafiki ambapo ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Pamba Fc kabla ya kuichapa Toto Africans mabao 3-0
Zahera amesema michezo hiyo ilikuwa maalum kuangalia ni kwa kiasi gani wachezaji wake wameiva baada ya mazoezi waliyofanya