Nembo ya Mdhamini wa ligi Kuu ya Tanzania Bara, kampuni ya Vodacom, imepambwa kwa rangi nyekundu na nyeupe
Bodi ya Ligi imetoa maelekezo kwa timu zote kuweka nembo hiyo katika jezi zao bila ya kuifanyia marekebisho
Ikumbukwe miaka ya nyuma Yanga ilitumia nembo maalum ya Vodacom iliyokuwa na rangi za njano na kijani
Uongozi wa Yanga umesisitiza kuwa hauko tayari kutumia rangi nyeupe na nyekundu kwenye jezi zao kwa kuwa sio rangi rasmi za klabu hiyo
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema rangi rasmi za Yanga ambazo zinatambuliwa na TFF ni kijani, njano na nyeusi
Hivyo hawatarajii TFF kuwalazimisha kutumia rangi ambazo haziko kwenye katiba yao
"Tuna rangi tatu ambazo ni kijani, njano na nyeusi, TFF wenyewe walishatupitishia hilo kwa hiyo tutashangaa watakapokuwa wanatuletea rangi ambayo hatujaipitisha sisi"
"Msimamo wetu ni kwamba wawaombe wadhamini, tunawaheshimu, tunawapenda na tunawahitaji..Hata kama tuko kwenye matatizo ya kiuchumi lakini hali hiyo isitumike kama kichocheo cha kututaka tubadili Katiba yetu"
"Katiba yetu haituruhusu kuvaa rangi nyekundu"