Kati Septemba 13-15 Yanga itashuka kwenye uwanja wa Taifa kuumana na ZESCO United kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa, raundi ya kwanza
Kama Yanga itacheza na ZESCO Septemba 15, siku tatu baadae italazimika kusafiri mkoani Mbeya kuikabili Mbeya City kisha kusubiri siku nyingine tatu kuikabili Tanzania Prisons Septemba 21
Baada ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, Yanga inapaswa kusafiri nchini Zambia ambako Septemba 26 itarudiana na ZESCO
Ni dhahiri kama ratiba hii haitafanyiwa marekebisho hasa kwa michezo ya ligi kuu, itakuwa adhabu kwa wachezaji kwani watacheza wastani wa mechi nne katika kipindi cha siku 10
Wakati msimu uliopita Simba ilipewa mazingira mazuri ya kuhakikisha wanafanya vizuri michuano ya ligi ya mabingwa, itakuwa jambo la kushangaza kama Bodi ya ligi itashindwa kuipa mazingira kama hayo Yanga
Haimaanishi kwa kuwa Simba alipewa mapumziko ya hadi mwezi mzima kwenye ligi ili wajiandae na michezo ya ligi ya mabingwa, basi na Yanga apewe hivyo
Mfano baada ya kucheza na ZESCO jijini Dar es salaam, ingefaa Yanga iachwe ijiandae na mchezo wa marudiano utakaopigwa nchini Zambia siku 10 baadae
Lakini kucheza mechi mbili za ligi kisha kuelekea Zambia kurudiana na ZESCO katika mchezo ambao unatarajiwa kuwa mgumu, hakutaisaidia Yanga wala Tanzania kufanya vizuri kwenye michuano hiyo