Kulingana na ratiba ya CAF, mchezo wa raundi ya kwanza ya michuano ya ligi ya mabingwa kati ya Yanga dhidi ya ZESCO utapigwa kati ya Septemba 13-15
Kama ilivyokuwa kwa Rollers, Yanga itaanzia nyumbani mchezo wa kwanza kisha kwenda kumaliza kazi nchini Zambia kati ya Septemba 27-29
Mchezo huo utawakutanisha walimu wenye historia tofauti
Kocha Mwinyi Zahera alitua kuinoa Yanga baada ya George Lwandamina kuondoka kwenda kujiunga na ZESCO United
Lwandamina atarejea tena Tanzania lakini sasa akiwa mpinzani wa Yanga, timu aliyonoa kwa msimu mmoja na nusu na kuipa ubingwa wa ligi kuu
Jambo zuri hapa ni kuwa benchi la ufundi la Yanga litakuwa na taarifa sahihi kuhusu aina ya uchezaji wa Lwandamina
Aidha Noel Mwandila aliyeletwa nchini na Lwandamina, atakuwa na jukumu la kuhakikisha bosi wake huyo wa zamani hatoki salama na timu yake watakapokuja nchini
Ukiangalia benchi la ufundi la Zahera ni wale wale waliofanya kazi na George Lwandamina isipokuwa kocha wa makipa Peter Manyika aliyechukua nafasi ya Juma Pondamali