Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Dismas Ten amesema benchi la ufundi la timu hiyo liliomba michezo miwili ya kirafiki waliyocheza dhidi ya Polisi Tanzania na AFC Leoprads na si kweli kwamba uongozi wa timu hiyo uliandaa wenyewe
Akizungumzia kauli aliyotoa kocha Mwinyi Zahera juzi baada ya mchezo dhidi ya AFC Leopards, Ten amesema wao kama viongozi wasingeweza kuandaa michezo ya kirafiki bila ya benchi la ufundi kupendekeza
Juzi Zahera alikosoa ziara ya mikoa ya Kilimanjaro na Arusha ambapo alisema haikuisaidia timu yake kwa kuwa walicheza kwenye viwanja vibovu huku wakikosa sehemu nzuri za kufanyia mazoezi
"Viongozi hatuwezi kutengeneza mechi bila ya benchi la ufundi kuomba," amesema
"Nakumbuka baada ya mchezo wa Township Rollers hapa nchini, benchi la ufundi waliomba kuwepo kwa mechi za kirafiki, mchezo mmoja wa ndani na mchezo mmoja wa Kimataifa ili kuweka timu sawa kuondoa yale makosa ambayo yalijitokeza kabla ya mchezo wa marejeano kule Gaborone Botswana"
"Kwa hiyo niseme tu kwamba, hakuna ambacho kimefanyika nje na muongozo wa benchi la ufundi, kitu pekee ambacho naweza kusema ni kwamba, sisi tunaamini kwamba Michezo hii miwili imeleta picha nzuri zaidi kwenye benchi la ufundi ili kuweza kuiweka timu sawa na kwenda kujiandaa kwa ajili ya mchezo wa marejeano Botswana"
Kikosi cha Yanga tayari kiko Botswana kikiendelea na maandalizi kuelekea mchezo huo ambao utapigwa Jumamosi, August 24