Klabu ya Yanga imewataka wanachama na mashabiki wake kununua jezi halisi za klabu hiyo ambazo zina nembo ya Mdhamini, kampuni ya GSM
Baada ya wajanja kuitumia nembo ya Yanga kwa miaka mingi kujinufaisha kupitia mauzo ya jezi, msimu huu uongozi wa Yanga umejipanga kuhakikisha klabu inanufaika na mauzo ya jezi
Akiwa mkoani Arusha juzi, Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla aliwataka wadau wa Yanga kununua jezi halisi ili kuichangia timu hiyo
Alisema jezi zinazotolewa na GSM zina ubora wa hali ya juu na itakuwa rahisi kwao kubaini jezi feki ambapo pia aliwataka kutoa taarifa Polisi au kwa uongozi wanapobaini kuwepo kwa watu wanaouza jezi hizo bandia
Mpaka sasa mauzo ya jezi za Yanga yanakwenda vizuri changamoto ikibaki kwa kampuni ya GSM ambayo bado haijajipanga sawasawa kwendana na mahitaji ya soko
Kila shehena ya jezi inapoingia sokoni inamalizika baada ya muda mfupi
Hata hivyo GSM imeahidi kutatua changamoto hiyo ambapo hivi karibuni mzigo mkubwa wa jezi utaingia
Juzi DK Msolla alisema jezi hizo zitauzwa kwa bei ya chini kidogo ambayo ni Tsh 30,000/- na 20,000/-tofauti na mwanzo ambapo jezi ziliuzwa Tsh 35,000/- na Tsh 30,000/-