Kiungo Mohammed Issa 'Banka' ameuanza vyema msimu kwa kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Mwinyi Zahera
Katika michezo miwili ya ushindani ambayo amecheza mpaka sasa, Banka 'amekichafua' vilivyo
Achilia mbali umahiri wake wa kupiga pasi, Banka ameonyesha uwezo mkubwa wa kupanda na kushuka kusaidia safu ya ulinzi pale timu inaposhambuliwa
Ameonyesha maelewano mazuri sana katikati akiwa na nahodha Papy Tshishimbi
Ubora huo alioanza nao, unawaweka viungo wengine kwenye wakati mgumu wakiwemo Feisal Salum 'Fei Toto', Abdulaziz Makame na Raphael Daudi
Fei Toto hakuwa na mpinzani msimu uliopita, lakini ni dhahiri msimu huu atapaswa kufanya kazi ya ziada kupata nafasi mbele ya nduguye huyo kutoka visiwani Zanzibar
Makame bado hajaweza kupata muda wa kutosha kwenye kikosi cha Yanga (alifanya mazoezi kwa siku chache Morogoro na baadae kujiunga na timu ya Taifa) lakini ni kiungo anayeweza kutoa changamoto
Ushindani huo wa namba utainufaisha zaidi Yanga kwani yeyote atakayepata nafasi ya kuanza, atataka afanye vizuri ili aendelee kuwa chaguo la kwanza
Kocha Zahera sasa ana kikosi kipana ambapo anaweza kupanga timu yake kufuatana na mahitaji ya mchezo
Kwani karibu kila nafasi ina angalau wachezaji wawili ambao wana uwezo unaokaribiana