Kuna utofauti mkubwa sana wa kikosi kilichocheza mchezo dhidi ya Township Rollers mwaka jana na hiki kilichosukwa upya na kocha Mwinyi Zahera
Nahodha Papi Tshishimbi na Kelvin Yondani ndio wachezaji pekee ambao walikuwemo kwenye kikosi kilichopoteza mchezo kwa kufungwa 2-1 mwaka jana
Pengine ni Tshishimbi pekee ambaye anaweza kuwemo kwenye kikosi cha Yanga kesho
Aidha chini ya Zahera, Yanga pia imebadili aina ya uchezaji wake ambapo wachezaji wapya wameonesha kuelewa mbinu za Mcongomani huyo haraka
Ni mbinu hizo hizo Zahera alitumia msimu uliopita lakini mara kadhaa alilalamika kuwa hakuwa na wachezaji wa kuweza kufanya kile alichotaka, sasa anao
George Lwandamina aliyeiongoza Yanga kwenye mchezo wa mwaka jana, alipendelea zaidi mbinu ya kujihami 'kupaki basi' na kutumia mashambulizi ya kushitukiza
Mbinu hiyo ndio iliwapa Rollers mwanya wa kutawala mchezo na kufanya walivyotaka mwaka jana
Zahera ni muumini wa 'total-football' ambapo wachezaji wanajilinda na kushambulia pamoja
Silaha kubwa ya mbinu hiyo ni wachezaji wenye kasi ambao wataweza kuharakisha mashambulizi langoni kwa timu pinzani pale wanapounasa mpira
Mechi dhidi ya Kariobangi Sharks Yanga walitumia mbinu hiyo na kama washambuliaji wake wangekuwa makini, wangefunga zaidi ya mabao matatu kwenye kipindi cha kwanza
Kesho Rollers wanaweza wasiwe na nafasi ya kutawala mchezo kama walivyofanya mwaka jana kwa kuwa Yanga itakuwa na watu wengi nyuma ya mpira
Lakini pia, walinzi wa timu hiyo watakuwa na kazi ya kudhibiti mashambulizi ya Yanga ambayo yatakuwa yakitoka kila upande
Aidha wingi wa mashabiki wa Yanga uwanjani, ni silaha nyingine muhimu ambayo itaweza kuwasaidia mabingwa hao wa kihistoria kupata ushindi nyumbani