Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera ana kila sababu ya kutembea kifua mbele baada ya kuongeza watu wa maana kwenye safu yake ya ulinzi
Wachezaji wote watano waliosajiliwa kuongeza nguvu kwenye safu hiyo, wameonyesha uwezo mkubwa mazoezini
Hapa nawazungumzia Lamine Moro, Ally Mtoni, Mustapha Suleyman, Ally Ally na Mwarami Issa 'Marcelo'
Wakati Lamine, Mtoni na Mustapha wakitamba kwenye nafasi za ulinzi wa kati, Ally Ally na Marcelo wameonyesha uwezo mkubwa wa kucheza beki wa pembeni
Aidha Cleofas Sospeter ambaye alipandishwa kikosi cha kwanza msimu uliopita na kocha Zahera, nae amekuwa kama ingizo jipya kutokana na uwezo mkubwa anao onyesha
Pengine hii ndio sababu uongozi wa Yanga hauna habari na akina Yondani, Abdul na Dante ambao inasemekana wameweka mgomo wakishinikiza walipwe madai ya fedha za miaka ya nyuma
Mabeki hao hawakuripoti kambini mkoani Morogoro kujifua na wenzao
Katika michezo mitatu ya kirafiki ambayo Yanga imecheza mpaka sasa mkoani Morogoro, kocha Noel Mwandila amewatumia 'walinzi pacha', Lamine/Cleofas, Mtoni/Cleofas, Mtoni/Mustapha, Lamine/Mtoni na Lamine/Mustapha huku Ally Ally na Marcelo wakitamba pembeni