Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga Frank Kamugisha amesema timu hiyo kwa sasa imeweka kambi mkoani Morogoro kutokana na ushauri wa kitaalam waliopewa na sio kwa sababu hawana fedha
Akizungumza alipotembelea kambi ya Yanga mkoani Morogoro mapema leo, Kamugisha amesema kambi ya Morogoro ni mwanzo tu ambapo timu hiyo itaweka kambi nje ya nchi wakati itakapoanza kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa kutegemeana na timu watakayopangiwa nayo
"Morogoro tunaanzia kama alivyosema Engineer na Mzee Manara hapa, baada hapo Yanga yetu hii tukishapangiwa timu na CAF ya kucheza nayo, tutakwenda kuweka kambi katika nchi ambayo mazingira yake yataendana na hiyo nchi ambayo tutapangiwa kwenda kucheza," amesema
"Nia yetu Yanga sio kutaka kujionyesha kwani kama uwezo tunao, nia tunayo lakini tunafuata ushauri wa kitaalam juu ya nini kifanyike wakati gani, kwa muda gani na kwa jinsi gani"
"Kwa hiyo Yanga Africans imeanzia kambi Morogoro lakini safari ya kwenda kuweka kambi sehemu inayotakikana kulingana na mazingira huo ndio utakuwa utaratibu wa Yanga yetu wakati inashiriki michuano ya Kimataifa"
"Tutaweka kambi kwenye mazingira sawasawa na nchi tunayokwenda kucheza, hatufanyi mchezo mchezo"