Beki mpya wa Yanga Ally Mtoni 'Sonso' amesema anapaswa kufanya mazoezi kwa bidii na kujituma ili kuweza kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo
Mtoni alijiunga na kambi ya Yanga hivi karibuni baada ya kumaliza mapumziko kutokana na ushiriki wake katika michuano ya Afcon 2019 na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania
Hata hivyo amesema muda mfupi aliofanya mazoezi na wachezaji wenzake, amebaini Yanga ya sasa imejaa wachezaji wenye vipaji na haitakuwa kazi rahisi kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza
"Hii ni timu kubwa tofauti na ninapotoka kila mchezaji hapa ana ubora mkubwa sana hasa timu hii ya sasa, kupata kwangu nafasi ya kucheza ni kujituma tu hakuna lingine kuanzia mazoezini mpaka kwenye mechi," amesema
Mtoni ni miongoni mwa wachezaji wapya waliotua kuongeza nguvu kwenye safu ya ulinzi ya kikosi cha Yanga
Wachezaji wengine waliosajiliwa kwenye safu hiyo ni Lamine Moro, Mustapha Suleyman, Muharami Issa 'Marcelo' na Ally Ally
Walinzi hao wanaungana na Kelvin Yondani, Andrew Vicent, Cleofas Sospeter, Paulo Godfrey 'Boxer' na Juma Abdul