Mlinda lango mpya wa Yanga Farouq Shikalo anasubiri michuano ya Afcon 2019 inayoendelea huko Misri imalizike ili ajiunge na mabingwa hao wa kihistoria
Kulingana na gazeti la Mwanaspoti, juzi Shikalo alikutana kwa mara nyingine na kocha Mwinyi Zahera ambapo pamoja na mambo mengine, mlinda lango huyo wa Harambee Stars alipendekeza majina ya wachezaji wawili ambao anaamini wanaweza kuifanya Yanga iwe moto wa kuotea mbali msimu ujao
Kulingana na gazeti hilo, Shikalo alimkabishi Zahera majina ya Patrick Kaddu na Umar Kasumba.
Kaddu ndiye aliyewafunga DR Congo bao la kwanza wakati timu ya Taifa ya Uganda ‘The Craines’ ikishinda mchezo wake wa kwanza kwenye fainali za Afcon
Katika mchezo huo The Craines ilishinda mabao 2-0 huku Kaddu anayekipiga KCCA ya Uganda, akifunga bao la kwanza kwa kichwa kuunganisha mpira wa kona.
Kwa upande wake, Kasumba ndiye mshambuliaji tegemeo kwenye kikosi cha Sofapaka (Batoto ba Mungu) kinachoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL).
Hata hivyo, Shikalo alimpongeza Zahera kwa kufanya usajili wa straika wa Polisi ya Uganda, Juma Balinya akisema Yanga imelamba dume kwani Mganda huyo ni hatari anapokaribia lango la adui.
"Nimekutana na mwalimu na amezungumza mambo mengi, lakini nilimweleza mawazo yangu kuhusu washambuliaji wawili wa Uganda ambao nawafahamu vizuri. Wanacheza Ligi Kuu Kenya.
"Pale Kenya kuna mtu anaitwa Umar Kasumba anachezea Sofapaka, huyu anajua sana kuwasumbua mabeki na juzi hapa Misri nimemuona huyu aliyewafunga Congo bao la kwanza anaitwa Kaddu (Patrick) ni mzuri sana.
"Ila kocha ameniambia kuwa atalifanyia kazi hilo japo tayari mabosi wake wamemsajili mshambuliaji aliyeongoza kwa ufungaji pale Uganda, nadhani na huyo atakuwa bora zaidi kwa rekodi hiyo.
"Kwa upande wangu niko vizuri na tutamalizana na Yanga muda si mrefu, kwa sasa nataka hizi fainali zimalizike kwani nimeamua kutafuta changamoto nyingine. Nahitaji kuondoka Kenya kwa sasa," alisema Shikalo