Wakati tetesi kuhusu usajili wa kiungo James Kotei zikizidi kupamba moto, uongozi wa Yanga umezikana taarifa zinazosambaa kuwa umemsajili kiungo huyo aliyemaliza mkataba kunako klabu ya Simba
Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema wamemaliza kufanya usajili wa nyota wa kigeni, kwa hiyo taarifa hizo hazina ukweli wowote
"Sisi tmeshamaliza usajili wa nyota wa kigeni, kwa sasa tunashughulika na nyota wazawa na wale waliomaliza mikataba ambao wamependekezwa kuendelea kubaki nasi," amesema
"Kama kutakuwa na usajili wa nyota mwingine wa kigeni, sifahamu kocha Mwinyi Zahera ndiye anayependekeza nani asajiliwe, sina taarifa kama alimpendekeza kiungo huyo"
Yanga imekamilisha usajili wa nyota nane wa kigeni huku ikimuongeza mkataba kiungo Papi Tshishimbi wakati mlinda lango Klaus Kindoki bado ana mkataba wa mwaka mmoja
Kumekuwa na sintofahamu kuhusu hatma ya Kindoki licha ya uongozi wa Yanga kusisitiza mlinda lango huyo ataendelea kubaki Jangwani
Kama mkataba wake utavunjwa basi Yanga itakuwa na nafasi ya kusajili nyota mmoja wa kigeni