Licha ya kutojumuishwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda kinachoshiriki fainali za Afcon 2019 nchini Misri, mshambuliaji Juma Balinya ni miongoni mwa wachezaji wanaotikisa soka la Uganda kwa sasa
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Polisi Fc, Juni 15 alisaini mkataba wa miaka miwili kuwatumikia mabingwa wa kihistoria, Yanga
Balinya ambaye alikuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Uganda msimu uliopita akifunga mabao 19 kwenye mechi 24, atatumia jezi namba 9
Maisha yake ya soka nchini Uganda aliyaanza katika klabu ya Vipers Fc kisha kuelekea Djibout kujiunga na AS Port ambako alicheza kwa miaka miwili
Baada ya kurejea Uganda, aliitumikia Lweza Fc kwa muda mfupi kabla ya kujiunga na Polisi Fc msimu wa 2017/18
Ni katika klabu hiyo ya Polisi ndipo alipojijengea heshima na kupata jina ambapo timu kadhaa zilijitosa kumuwania kabla ya Yanga kufanikiwa kuinasa saini yake akiwa njiani kujiunga na Simba
Waganda wengi wanaamini Balinya atapata mafanikio makubwa katika klabu ya Yanga kama ilivyokuwa kwa Mganda mwingine Emmanuel Okwi aliyepata mafanikio na klabu ya Simba