Yanga imealikwa kushiriki michuano ya CECAFA Kagame Cup itakayofanyika mwezi ujao kuanzia Julai 07 mpaka Julai 21 nchini Rwanda
Hata hivyo bado haijathibitisha kama itashiriki michuano hiyo au la
Mwaka jana Yanga haikushiriki michuano hiyo ilipofanyika jijini Dar es salaam viongozi wa timu hiyo wakiwapa mapumziko wachezaji wao
Tayari watani zao Simba wametangaza kutoshiriki michuano ya mwaka huu wakitaja sababu ya muingiliano wa ratiba na kambi yao
Yanga na Simba zitashiriki michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao, na mwaka huu michuano hiyo hatua ya awali itaanza mapema tu mwanzoni mwa mwezi wa nane
Ratiba ya michuano ya Kagame imeingiliana na ratiba ya michuano ya AFCON inayoanza kutimua vumbi nchini Misri Juni 21 na kumalizika Julai 19
Ni dhahiri kama Yanga itashiriki michuano hiyo, itawakosa wachezaji wake ambao wako kwenye timu za Taifa huko Misri
Idadi kubwa ya wachezaji wapya waliosajiliwa na Yanga watakuwa Misri na timu zao za Taifa
Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Omary Kaya amesema wanafanya tathmini kabla ya kuamua kama washiriki au la
Uongozi wa Yanga umeweka wazi malengo yao ya kuweka kambi nje ya nchi kujiandaa na mashindano ya msimu ujao
Kambi hiyo huenda ikawa mwezi wa saba hivyo nao wanaweza kukabiliana na changamoto ya muingiliano wa ratiba
Baada ya kusajiliwa wachezaji wengi wapya, Yanga inahitaji angalau wiki tano kuwaweka wachezaji pamoja ili wazoeane