Yanga ndio timu iliyo 'busy' zaidi kwenye soko la usajili msimu huu ikiendelea kumalizana na nyota kadhaa watakaoitumikia msimu ujao
Baada ya kukamilisha usajili wa wazawa watatu, mzawa mwingine anayetajwa kusaini Jangwani ni mshambuliaji wa Ndanda Fc, Vitalis Mayanga
Mmoja wa viongozi wa Yanga aliyeko kwenye Kamati ya usajili ya timu hiyo amethibitisha kusajiliwa kwa mshambuliaji huyo aliyeifungia Ndanda Fc mabao 10 kwenye ligi iliyomalizika
"Ndio, tumemsajili kama mchezaji huru, mkataba wake na Ndanda FC umeshamalizika, sasa rasmi Mayanga ni mchezaji wa Yanga, amesaini miaka miwili," alisema kwa kifupi kiongozi huyo.
Ukimuondoa kiungo Abdulaziz Makame ambaye picha zilisambaa zikimuonyesha akisaini mkataba, wachezaji wengine wazawa wanaotajwa kusaini mikataba kimyakimya ni mlinda lango Metacha Mnata na beki Ali Mtoni ambao wote wako timu ya Taifa
Yamuwania straika kutoka Namibia
Yanga pia iko mbioni kukamilisha usajili wa mshambuliaji kutoka Namibia, Sadney Urikhob
Mshambuliaji huyo ambaye yuko katika kikosi cha timu ya Taifa ya Namibia inayojiandaa na fainali za AFCON 2019, alitarajiwa kuwasili jana kusaini mkataba kisha kurejea kwenye kambi ya timu ya Taifa
cutUrikhob alifanya majaribio katika klabu ya Simba na alicheza michuano ya Sportpesa Super Cup pamoja na beki Lamine Moro ambaye tayari ameshamwaga wino Jangwani

Beki kutoka Burundi asaini miaka miwili
Beki Mustapha Suleyman anayekipiga klabu ya Aigle Noir, mabingwa wa Burundi inaelezwa tayari amesaini mkataba wa miaka miwili
Mustapha ambaye anaweza kutumika kama kiraka kwa kuwa anaweza kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, aliwasili juzi usiku kumalizana na uongozi wa Yanga
Beki huyo pia yuko kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Burundi itakayoshiriki fainali za AFCON 2019 baadae mwezi huu
Nyota wakigeni waliosajiliwa wako saba
Mpaka sasa idadi ya nyota wakigeni ambao wamesajiliwa (wamesaini mikataba) wako saba ambao ni Farouq Shikalo (Kenya), Lamine Moro (Ghana), Issa Birigimana (Rwanda), Patrick Sibomana (Rwanda), Kalengo Maybin (Zambia), Mustapha Suleyman (Burundi) na Papi Tshishimbi aliyeongeza mkataba
Yanga bado ina nafasi tatu za kusajili wachezaji wa kigeni moja ikiwa ya Klaus Kindoki ambaye bado ana mkataba na mabingwa hao wa kihistoria
Mikataba ya nyota wengine wa kigeni waliokuwa wakiitumikia Yanga msimu uliomalizika, Amissi Tambwe na Thabani Kamusoko imemalizika na hakuna mazungumzo yaliyofanyika kuhuisha mikataba yao