Wachezaji wa zamani wa Yanga wamemtaka Mwenyekiti mpya, Mshindo Msolla, kutorudia makosa yaliyofanyika nyuma na kuchagua watu wasiofaa katika kamati mbalimbali ambazo zitaundwa na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.
Mmoja wa wakongwe hao ni beki wa kushoto, Anwar Awadh ambaye alimshauri Msolla kuwaweka watu wa mpira na kuachana na wale ambao hawataweza kuisaidia Yanga.
“Kama kuna kosa kubwa atalifanya Mwenyekiti ni kuwarudisha tena wapigaji walioikosea heshima klabu, ni vyema kuwafungia vioo kabisa na kuchagua watu watakaojali timu kuliko maslahi yao,” alisema Awadh.
Kwa upande wa Ramadhan Kampira, alisema si jambo zuri hata kidogo kuwarudisha viongozi ambao tayari zama zao zilipita kwa timu hiyo yenye historia kubwa hapa nchini.
“Nimesikia kuna kamati ndogo ndogo zinataka kuundwa, nimpe tu angalizo Mwenyekiti(Msolla), asije kujichanganya kuwarudisha wapiga dili kwa kuwa watairudisha timu nyuma,’’ alisema Kampira.
Naye shabiki wa timu hiyo, Abdulmalik Hussein, alisema jambo pekee ambalo Yanga wanaweza kumkumbuka Msolla ni kuitendea haki nafasi yake ya uenyekiti pasipo kushikwa masikio na mtu.
“Timu ilipoteza mvuto matajiri waliikimbia kutokana na viongozi waliopita walikuwa si watu wa soka, sasa tunaomba asiwarudishe tena awapotezee kabisa,’’ alisema Abdulmalik.
Akizungumzia juu ya mawazo hayo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, alisema wao kama viongozi wanajua wanachokifanya baada ya kupewa dhamana ya kuongoza jahazi la timu hiyo.
“Nikuhakikishie tu sisi hatutafanya kazi kwa kumwangalia mtu na wote tunawajua kwa sura hata majina na hakuna hata mmoja atakayepata nafasi kurejea tena,’’ alisema Mwakalebela