Wakati Mwanachama wa Yanga leo wakiwa na tukio muhimu la kuchagua viongozi wapya wa klabu hiyo, kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria kiko mkoani Iringa kikiendelea na maandalizi ya mchezo wa nusu fainali kombe la FA dhidi ya Lipuli Fc
Mchezo huo utapigwa kesho Jumatatu katika uwanja wa Samora
Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema mchezo huo una umuhimu wa kipekee kwa kikosi chake kwani wanahitaji kutwaa taji la FA ili kujihakikishia nafasi ya kurejea kwenye michuano ya Kimataifa msimu ujao
"Tunaendelea na maandalizi vizuri. Wachezaji wako na hali nzuri, tunahitaji kushinda ili tuweze kuingia fainali. Tumeendelea kurekebisha makosa tuliyoyaona mchezo dhidi ya Prisons ili tuwe vizuri zaidi mchezo dhidi ya Lipuli," amesema
Matumaini ya Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu yamezidi kufifia baada ya Simba kuendelea kushinda michezo yake ya viporo
Kama Simba itashinda mchezo wa leo dhidi ya Prisons, itafikisha alama 78 na kuwa alama mbili nyuma ya Yanga inayoongoza ligi ikiwa na alama 80 wakati huo huo Simba ikiwa bado na michezo minne ya viporo
Nafasi pekee ya Yanga kurejea kushiriki michuano ya CAF msimu ujao, imebebwa na ubingwa wa kombe la FA
Kama Yanga itafanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya Lipuli Fc kesho, itacheza na Azam Fc kwenye mchezo wa fainali utakaopigwa uwanja wa Ilulu mkoani Lindi Juni 02 2019