Winga wa KMC Hassani Kabunda amesema yuko tayari kujiunga na Yanga kama atafikia makubaliano na uongozi wa timu hiyo
Kabunda ni mmoja wa wachezaji ambao wametupiwa jicho na Kocha Mwinyi Zahera aliyedhamiria kukisuka upya kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao
Winga huyo mwenye kasi anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji waliopendekezwa na Zahera kwa ajili ya kuwatumikia mabingwa hao wa kihistoria
"Mimi sina tatizo kucheza Yanga. Muhimu viongozi wafuate taratibu zote za usajili, tukikubaliana nitasaini kwani ili niendelee kuwa na kiwango bora cha soka ni lazima nipate changamoto ya kuichezea timu kubwa kama Yanga," amesema
Yanga imedhamiria kukamilisha michakato yote ya usajili mwezi huu kabla ya Zahera kurejea DR Congo katika kikosi cha timu ya Taifa ambacho mwanzoni mwa Juni kitaanza maandalizi ya michuano ya AFCON 2019
Yanga inaendelea na michakato yake ya usajili kwa usiri mkubwa kuhakikisha haikumbani na changamoto ya kunyan'ganyana wachezaji na Simba ambayo msimu uliopita iliwasajili wachezaji wengi waliokuwa wakiwaniwa na Yanga licha kutowatumia baadhi ya wachezaji hao