Mgombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela amesema anataka kuifanya klabu hiyo kuwa tofauti na miaka yote.
Akizindua kampeni yake katika makao makuu ya klabu hiyo leo, Mwakalebela alisema iwapo ataingia katika katika uongozi ataifanya Yanga kupata fedha kupitia rasilimali za klabu.
"Nikipata nafasi ya kuingia katika uongozi tutakuwa na utaratibu maalum wa michango ili kujua tuna wanachama wapi kwa wingi, pia jinsi ambavyo wanachanga basi fedha hizo ziende sehemu sahihi,” alisema.
Mwakalebela alisema yeye pia ni muumini wa kutaka mabadiliko katika klabu hiyo, hivyo akifanikiwa kuingia atahakikisha wanaingia katika mabadiliko.
"Tukifanikiwa kuingia tutaitisha mkutano mkuu na wanachama na kujadiliana ili kupitisha utaratibu maalum wa kufanya mabadiliko," alisema katibu huyo wa zamani TFF.
Akizungumzia kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema amekuwa akifurahishwa na jinsi ambavyo anaishi na wachezaji wake hivyo kama akifanikiwa kuingia atamuongezea cheo cha umeneja huku akisaidiana na wasaidizi wake pamoja na walimu kutoka timu za vijana.
"Zahera ni zaidi ya mwalimu, baba katika timu yetu amekuwa akiishi nao vizuri na kuifanya timu yetu kupambana mpaka hivi sasa."